Chama cha Wasafirishaji wa Mafuta Tanzania (Tatoa), kimesema Rwanda na
Uganda zitajitoa kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuanzia Septemba Mosi,
mwaka huu.
Katibu Mtendaji wa Tatoa, Zacharia Hanspope aliwaambia waandishi wa
habari jana baada ya kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti
kuwa nchi hizo zinajitoa kutokana na matatizo mbalimbali ambayo kwa muda
mrefu zimekuwa zikiyalalamikia lakini Serikali haikuchukua hatua.
Hanspope alisema ushuru wa barabara na ushuru wa forodha ni baadhi ya
vikwazo ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa kwa muda mrefu na
wafanyabiashara mbalimbali wa nchi hizo.
“Serikali ipunguze gharama za ushuru wa barabara na ushuru wa forodha
ili kuwa na ushindani sawa na bandari nyingine na hivyo kuzivutia
kutumia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Hanspope.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Omary Chambo alikataa kuzungumzia
lolote kuhusu suala hilo akisema halina mantiki yoyote kwake.... “Hivi
hilo jambo unaloniuliza lina sense (mantiki) yoyote? Mie siwezi kujibu
lolote nenda ukamuulize mwenyewe (Hanspope) maana wakati akisema mimi
sikuwepo.”
Alisema kujitoa kwa Rwanda na Uganda kuitumia Bandari ya Dar es Salaam
hakutakiathiri chama hicho tu, bali uchumi wa taifa kwa ujumla.
Hayo yanatokea wakati Rwanda ikiendeleza vita yake ya maneno na Tanzania
na mfululizo wa matukio ya kuitenga Tanzania kwenye Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Viongozi wa Kenya, Rwanda na Uganda walikutana Juni 25, mwaka
huu mjini Entebbe, Uganda na kukubaliana kuongeza uhusiano wa
kibiashara baina yao.
Kamati ya Bajeti:
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge alisema
katika kikao kijacho cha Bunge, kamati hiyo itaibana Serikali kuhusu
mikakati inayofanywa kukabiliana na ushindani wa kibiashara katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema sababu ya Rwanda na Uganda kujitoa kutumia Bandari ya Dar es
Salaam ni vikwazo katika barabara ikiwamo mizani mingi ya kupimia
mizigo.
“Mizani ni mingi pia kuna usumbufu katika kupima mizigo yao na kwamba
hali hiyo inawaletea usumbufu wafanyabiashara wengi,” alisema.
Alisema vitendo vya askari wa usalama barabarani kudai rushwa pia ni
miongoni mwa vikwazo pamoja na urasimu mkubwa katika utoaji wa mizigo
bandarini ikilinganishwa na bandari nyingine.
“Ni lazima tujifunze kwa majirani zetu Msumbiji, upanuzi wa haraka wa
Bandari ya Beira umekuwa kikwazo kwetu, kampuni nyingi zimeanza kuitumia
bandari hiyo,” alisema.
Chenge alikitaka chama hicho kuiandikia kamati hiyo mapendekezo yake
ikiwa ni hatua ya kunusuru uchumi wa nchi ili waweze kuijadili bungeni.
Umoja wa nchi tatu:
Marais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Paul Kagame wa Rwanda na mwenyeji wao
Yoweri Museveni walikutana mjini Kampala, Uganda na kuamua kuitumia
Bandari ya Mombasa kwa shughuli zao.
Waliahidi kuimarisha ufanisi katika huduma za Bandari ya Mombasa ili kuhakikisha bidhaa zinafika mapema Uganda na Rwanda.
Pia walikubaliana kujenga reli mpya ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka Mombasa kwenda Kenya na Uganda.
Viongozi hao walikubaliana pia kushirikiana katika sekta ya nishati hasa ikizingatiwa kuwa Uganda imegundua mafuta.
Nchi hizo tatu ambazo zimeruhusu kwa raia wao kusafiri kwa vitambulisho
pale wanapotembelea nchi tatu miongoni mwao, zitakutana tena Kenya mwezi
huu.
Source:Mwananchi
DJ NYASI24.COM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
-
Huyu ni msanii wa vichekesho akijulikana kama Kinyambe ambae ameonekana akijizolea umaarufu kutokana na staili yake anayoitumia kuigizia ...
No comments:
Post a Comment